Nakutana kwa mara ya kwanza na Herieth Paul na nagundua anaonekana ni mdogo kuliko nilivyokuwa nikimuona kwenye picha.
Mkononi amebaba lijititabu kubwa kama vile album ya picha. Ananiambia kuwa ni ‘portifolio’ iliyojumuisha baadhi ya picha zake bora kwaajili ya kuwaonesha wateja wa kazi yake.
Herieth Paul kwenye jarida la DuJour
Muda mfupi nagundua kuwa ni msichana mcheshi na mwepesi wa kuzoeleka. Tunaanza kuzungumza kwenye mahojiano maalum ya kipindi (podcast) yangu ambayo muda huo hata sijui nitaipa jina gani. Ni hivi karibuni tu nimepata jina lake na kuibatiza Chill na Sky. Unaweza kukisikiliza katika mfumo wa sauti tu hapo chini.
“Mimi nimezaliwa Muhimbili mwaka 1995,” anasema Herieth. “Nilianzia kusoma Chang’ombe, Keko pale nikasoma chekechea na darasa la kwanza kidogo, lakini sasa pale baba yangu alikuwa polisi kwahiyo tukahamia Mbagala. Nikafika Mbagala lakini nikawa bado nasoma shule Chang’ombe. Nikawa napanda basi kuanzia asubuhi kutoka kwenda Chang’ombe na usiku narudi peke yangu darasa la kwanza.”
Herieth (kulia) kwenye jarida la Harpers Bazaar UK la August 2014, models wengine ni Jiyoung Kwak na Helena Greyhorse
Anasema familia yao ilikuwa ya ‘kishua’ japo wazazi wake waliamua kuwalea watoto wao katika mazingira ya kawaida.
“Ningekuwa ni mtoto ambaye napata kila kitu nilipokuwa mdogo, nilipoanza kutengeneza hela nisingekuwa naweza kusave na kufanya vitu vikubwa,” anasema.
Herieth Paul kwenye jarida la Dress to Kill
Maisha ya Canada yalianza baada ya mama yake anayefanya kazi za ubalozi kuhamishiwa nchini humo ambapo ilibidi wahame wao wenyewe pamoja na dada yake na kumwacha baba yake aliyekuwa akiendelea na kazi.
Anasema maisha ya Canada yalikuwa magumu mwanzo kutokana na ugeni pamoja na baridi kali la nchini humo. “Nilitoka nje nikiwa na kandambali, miguu iliganda hivi. Nilipoondoka juzi juzi baridi lilikuwa ni -21 wakati mwingine huwa inafika hadi -45 huwa wanafunga kabisa maduka hauruhusiwi kutoka nje,” anakumbushia.
Herieth kwenye jarida la Glamour la Marekani, August 2014
Herieth anasema ndoto ya kuwa mwanamitindo ilikuja kama bahati tu kwakuwa mwanzoni alikuwa anapenda kuwa muigizaji. Baada ya kumsumbua sana mama yake, alipelekwa kwenye kile mama yake alichodhani ni chuo cha uigizaji lakini kumbe sio!
Anasema pamoja na kukosea njia na kwenda kwenye chuo cha masuala ya mitindo, wahusika waligundua kitu cha pekee kwake. “Mungu akapenda tukaendelea vizuri ndio nikafika New York. “Yule mama ambaye alinisaini pale Canada, Angies Model, alinipiga picha na simu yake, alipiga picha zikiwa na quality mbayaaaa akaziweka kwenye computer saa hiyo hiyo akazituma New York kesho yake nikaitwa,” anasema Herieth.
Herieth anadai haikuchukua muda tangia alipofika jijini New York, kazi kubwa zikaanza kumuijia huku kazi ya kwanza ilikuwa ni kuwekwa kwenye jarida la Italian Vogue.
Hadi sasa ametaja baadhi tu ya majarida makubwa ya fashion aliyotokea kuwa ni pamoja na Marie Claire, Dress to Kill, Vogue America, Teen Vogue, US Vogue, Glamour, Elle Netherlands na Canada na mengine.
Anaikumbuka siku aliyokutana na Naomi Campbell kuwa ilikuwa ya kipekee.
“Juzi mwezi wa September Naomi alikuwa backstage tumefanya naye show sikumuona mpaka ule muda wa show, nilipomuona nikaenda mpaka pale nikamuambia ‘Naomi you are so beautiful’ akasema ‘no wewe ndio mzuri’ nikasema ‘wewe ndio mzuri’. Lakini ni mama mzuri sana. Kwa vitu ambavyo amefanya kuanzia alivyokuwa na miaka 15 hadi sasa ana miaka karibia 45 amefungua uwezo wa sisi wasichana weusi kupata kazi ambazo tunapata sasa hivi.”
Herieth Paul kwenye jarida la Glass, 2014
Kanye West ni rapper anayemkubali mno.
“Nilikutana naye mara yangu ya kwanza backstage kwenye show ambayo tumeliza kufanya New York ilikuwa show ya designer mwingine. Alikuja show imeisha kila mtu anakimbia backstage kuvaa nguo kujaribisha nguo nikamuona amekuja nikakimbia nikamuita rafiki yangu. Kufika pale Kanye watu wamemzunguka ‘nikasema ohh my God nice to meet you’ akasema ‘good job umefanya kazi nzuri’ nikasema ‘whaat umeona show yangu kweli’ akasema ‘ofcourse’.
“Lakini mara ya pili kukutana naye nilifanya show yake 2012 alifanya show yake Paris. Backstage kama yupo kwenye creative process anafanya kazi, anafikiria anapiga nyimbo zake yaani anablast kwa nguvu kabisa. Ni mtu ambaye anapenda sana kazi yake, yuko passionate na kila kitu anachokifanya.”
Kwa upande mwingine nilitaka kujua anamchukuliaje Kendall Jenner, mdogo wake na Kim Kardiashian ambaye wamewahi kufanya kazi pamoja.
Kendall Jenner
“Mimi naona Kendall ana talent kabisa, kwasababu yule msichana ni mzuri kupita kiasi. Halafu ana proportion zote za kuwa model, ana urefu ana personality. Nimekutana naye tulikuwa casting za hiyo show ambayo tulipata amesubiri kwasababu kuna wasichana wengi ambao wanajipanga ili wawaone designers, kaja pale kasubiri kwenye mstari kama mtu yoyote. Hakusema ‘sijui mimi ni Kendall niingie wa kwanza’. Kakaa pale kimya tu, nikamwangalia akasema ‘hi’, yuko nice.”
Herieth Paul anasema anawekeza zaidi fedha zake kwenye ardhi na nyumba na tayari anamiliki mijengo kadhaa.
Home
»
» Unlabelled
» Alivyokutana na Naomi Campbell, Kanye West, Kendall Jenner, Calvin Klein, Tom Ford
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment