0
CHAMIWA Adamu (23), kijana ambaye ni mkazi wa Kilimahewa- Manzese jijini Dar, ameuawa kwa kuchomwa kisu cha shingo na mtu aliyetambulika kwa jina moja la Mpelu kisa kikidaiwa ni shilingi mia mbili tu!
Marehemu Chamiwa (pichani)alikuwa mwanafunzi mwenzake na staa wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwenye Chuo cha Magogoni, Dar.
 


Marehemu Chamiwa Adamu enzi za uhai wake.
Tukio la Chamiwa kuchomwa kisu lilijiri saa 11 jioni ya Machi 12, mwaka huu katika eneo lililofahamika kwa jina la Tishio, Manzese Midizini, Dar. 


SIKU YA TUKIO
Akisimulia mkasa huo mwanzo mwisho, mmoja wa wanafamilia ambaye hakupenda kutaja jina alisema, siku ya tukio, Chamiwa alikuwa na wenzake (hakuwataja majina), kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Mpelu alitokea na kumwomba shilingi mia mbili. 


“Marehemu alimwambia ana hela kubwa, kwa hiyo hana chenji, hivyo akamtaka amwache aende kutafuta chenji ili ampatie hiyo 200.“Ile anaondoka tu, Mpelu alimshika begani kwa nyuma, marehemu alipogeuka kumtazama, Mpelu akamchoma kisu sehemu ya shingoni. Palepale damu zikaanza kuchuruzika na marehemu akaanguka.
“Watu, akiwemo aliyemchoma kisu walimnyanyua marehemu na kumpakia kwenye gari iliyokuwepo pembeni ili kumpeleka Kituo cha Polisi Magomeni,” alisema mwanafamilia huyo.


KISU KILIVYOZAMA
Kwa mujibu wa mashuhuda, inadaiwa kuwa kisu alichochomwa Chamiwa, kilizama ndani ya mwili wake kwa umbali wa zaidi ya nchi mbili.
Simu ya marehemu. 


MTUHUMIWA ATAKA KUTOROKA
Habari zinadai kwamba, wakiwa njiani kumpeleka marehemu kituo cha polisi, mtuhumiwa huyo alibaini Chamiwa alishafariki dunia, akaomba afunguliwe mlango wa gari ili ashuke (kwa maana ya kukimbia) lakini wasamaria wema hao walimkatalia kwa vile walishtukia kwamba kesi ingekuwa yao, hivyo wakaongeza ulinzi kwa mtuhumiwa mpaka kituo cha polisi. 


WALIVYOSEMA MAJIRANI
Amani lilifanikiwa kufika nyumbani kwa marehemu na kuzungumza na baadhi ya majirani ambapo walisema Chamiwa alikuwa kijana mpole, mwenye kujituma na alikuwa hana shida kwa wenzake.“Tumeumia sana kusikia ameuawa kwa kuchomwa kisu. Tukimfikiria kijana wa watu alivyokuwa bado mdogo, maskini Chami! Amepoteza ndoto zake. Yeye ndiye aliyekuwa akishika nafasi ya baba mwenye nyumba kama mzee Adamu hayupo. Inauma! Ila tumuachie Mungu atamlipia,’’ alisema jirani mmoja.


SIMU YA MAREHEMU YAKUTWA NA DAMU
Amani lilifanikiwa kuiona simu aliyokuwa akiitumia marehemu enzi za uhai wake ikiwa imezimwa na kuchafukwa kwa damu iliyoganda.Mpaka juzi, mtuhumiwa huyo alikuwa bado anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Magomeni huku uchunguzi ukiendelea.
Staa wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’.


CHUONI KWA MAREHEMU
Amani lilifika kwenye chuo alichokuwa akisoma marehemu Chamiwa ambapo liliambiwa alikuwa mwaka wa kwanza akichukua masomo ya Information of Technology (IT).Mkuu wa wanafunzi (Dean of Students) aliliambia Amani kwamba, taarifa za mwanafunzi huyo kuuawa kwa kisu zimewafikia na wanachosubiri ni ratiba ya mazishi ili washiriki pamoja na familia.
“Kusema kweli tumepokea taarifa hizo lakini tunachosubiri ni ratiba ya mazishi ili na sisi tuweze kushiriki,” alisema mkuu huyo bila kutaja jina lake.
Wakati Amani linaondoka chuoni hapo liliwapa pole wanafunzi wenzake marehemu hasa wale wa mchepuo sanjari na wake, lakini pia lilimtafuta Lulu kwa lengo la kumpa pole lakini ilidaiwa kwamba, alishaondoka kurudi nyumbani.
Marehemu Chamiwa alizikwa Machi 13, mwaka huu mkoani Morogoro.
Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.

Post a Comment

 
Top