0

HAJAKOMA? Staa wa Bongo Fleva anayesumbua na wimbo wa Chumvini, Khaleed Mohamed ‘TID’ amehusishwa na msala mwingine baada ya kudaiwa ku kumjeruhi James Richard, mkazi wa Jiji la Dar.


 

Staa wa Bongo Fleva anayesumbua na wimbo wa Chumvini, Khaleed Mohamed ‘TID’. 

Endapo itathibitika kama ni kweli ametenda kosa hilo, TID atakuwa yupo katika hatari ya kuswekwa gerezani kwa mara ya pili kwani mwaka 2008 alitiwa hatiani kwa kosa la kumpiga Ben Mashibe, mkazi wa jijini Dar ambapo alifungwa jela mwaka mmoja kabla ya kuachiwa kwa msamaha wa rais.

Kwa mujibu wa chanzo kilichoshuhudia tukio hilo, TID anadaiwa kutenda kosa hilo maeneo ya Kinondoni-Sterio karibu na eneo analoishi ambalo amelipachika jina la Unyamani.Akizungumza kwa masikitiko, James alisema siku ya tukio, alifika maeneo hayo kukutana na rafiki yake, ghafla alitokea TID na kuanza kumsema vibaya kisha kumrushia makonde kwa madai kuwa aliegesha gari lake katika anga zake.
“Nilikuwa namsubiri mwenyeji wangu, ghafla alifika TID akiwa katika gari lake ambapo alikaa humo ndani ya gari kama dakika 30 na alivyoshuka alinisemea mbovu kisha kunivamia na kuanza kunipiga.


“Nikaishika cheni yake, akaivua na kuniachia kisha akaondoka. Baada ya muda alirudi akiwa amefuatana na kaka yake aliyefahamika kwa jina la Abdallah au Dulla Manga wakiwa wameshika visu. 


“TID akasema wewe ndiyo mwizi wangu wa cheni nipe cheni yangu haraka sana kabla sijakutoa nyama za makalio, alinivamia na kuanza kunishambulia kwa visu huku kaka yake akinishika ili kutoa nafasi kwa mdogo wake kunishambulia atakavyo,” alisema James. 


  Khaleed Mohamed ‘TID’. 


Alisema wakati anashambuliwa na TID, Dulla aliwaambia watu waliokuwepo kuwa wasiamulie na ambaye angekaidi angemchoma kisu cha chembe ambapo waliogopa mpaka alipofika mjumbe wa mtaani huo, akaamulia. 


Alisema kuwa TID alimpiga kiasi ambacho uso ulivimba, kuteguliwa mkono na kuchomwa visu kichwani na kisogoni ambako alitokwa damu nyingi hadi wasamaria wema walipoungana na mjumbe kumsaidia kisha kumkimbiza Kituo cha Polisi cha Oysterbay damu zikiwa zinamtoka chapachapa ambako alipata hati ya polisi ya matibabu (PF3) na kufungua kesi iliyosomeka OB/RB/3211/2013. 


Kitendo hicho kiliwakasirisha polisi waliokuwa zamu ambapo mmoja wao alisema anamshangaa TID kurudia kosa lililompeleka gerezani huko nyuma.James alisema baada ya kufungua kesi hiyo, alikimbizwa katika Hospitali ya CCBRT ambako alishonwa nyuzi nne katika jeraha la kisogoni na kupatiwa dawa kwa ajili ya maumivu ya mkono na usoni ambako alivimba sana. 


“Leo naenda (Jumanne) naenda tena hospitali ili nijaziwe PF3 yangu kwa ajili ya kulipeleka shauri hili mahakamani,” alisema James kwa masikitiko.Jitihada za kumpata TID anayesakwa na jeshi la polisi ili kusikia kauli yake kuhusiana na madai hayo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani.


Hata hivyo, waandishi wetu wanaendelea kumtafuta.

Post a Comment

 
Top