Wiki chache zilizopita mtangazaji Salma
Msangi wa 92.9 Magic FM kupitia kipindi cha Afrika Kabisa, alizungumza
kitu ambacho kiliwachoma wadau na wanamuziki wengi dansi – alisema
muziki wa dansi UMEKUFA!
Salma
akahoji ni vipi wao watangazaji waupige muziki ambao hautakiwi tena na
mashabiki. “Watu hawautaki tena muziki wa dansi …muziki wa dansi
umekufa,” alisikika mtangazaji huyo na kuwataka wasanii wa dansi waache
kulalamika na badala yake wasome alama za nyakati.
Katika
kusheresha kauli yake, Salma Msangi akampongeza Christian Bella kwa
kusoma alama za nyakati na kuamua kushirikiana na wasanii wa bongo fleva
kama Ommy Dimpoz na wengineo na sasa yuko juu.
Huo
ni mtazamo wa Salma Msangi na sitaki kuwa hakimu kwenye kauli yake –
anaweza kuwa sahihi au si sahihi, anaweza kuwa ametumia njia sahihi
kuzungumzia hilo lakini pia anaweza kuwa ametumia njia ya kuumiza na
kukatisha tamaa ila yote kwa yote hayo ni maoni ambayo yanapaswa
kufanyiwa kazi kwani pengine yapo mawili matatu yanayofaa katika safari
ya kuukwamua muziki wa dansi.
Kwangu
mimi naamini muziki wa dansi haujafa bali unazidi kukua kwa kasi ya
ajabu kiasi cha kujipenyeza kwenye aina nyingine ya muziki kama vile
bongo fleva, taarab na injili – ukifuatilia kwa makini aina hizo
nyingine za muziki utagundua kuwa kwa zaidi ya asilimia 40 wanautegemea
sana muziki wa dansi.
Majuzi
mwanangu wa kidato cha kwanza alinikuta natazama wimbo “Yarabi Nafsi”
wa Mapacha Watatu katika laptop yangu kupitia YouTube, akashangaa sana
na kuniuliza: “Hivi kumbe hata muziki wa bendi unapatikana You Tube?”
Nikamjibu kwa kumhoji: “Kwanini ulifikiri haupatikani?”.
Akanijibu:
“Kwa sababu najua watu hawapendi muziki wa bendi za dansi, hawatapata
viewers (watazamaji) wengi.” Kuthibitisha hilo akasogelea laptop yangu
na kuangalia wimbo umepata watazamaji wangapi \ akakuta 2781 akacheka na
kuniambia: “Si umeona watazamaji hao, sasa nenda kwenye video zingine
za bongo fleva au comedy uangalie ‘viewers’ utakuta ni elfu 50 na
kuendelea,”.
Kwa
bahati nzuri wakati dogo anayasema hayo nilikuwa na rafiki yangu aitwae
Sakala Jr tukatazamana na kutabasamu kwa uchungu, ulikuwa ni ukweli
unaoumiza kutoka kwa kijana mdogo ambaye ambaye anawakilisha sehemu ya
kizazi kikubwa kinachoamini kuwa muziki wa dansi kupitia bendi zetu
haukubaliki.
Na
ni hapo ndipo ninapojiuliza je bendi zetu zinajua kuwa zinahitaji
kuzalisha mashabiki wapya kwa maana ya kizazi kipya? Mashabiki wanazeeka
kiasi kwamba inafika wakati watu wanashindwa kwenda kwenye kumbi za
starehe, nani anaziba nafasi zao? Watangazaji na waandishi waliokuwa
wakiunadi muziki wa dansi miaka 20 iliyopita leo hii hawapo tena –
wengine wamestaafu, wengine wamefariki, wengine wamebadilishiwa majukumu
na sasa zimekuja damu mpya. Je bendi zetu zimefanya juhudi za
kuishawishi jamii mpya ya wana habari?
Wanamuziki
nao wanapotea mmoja mmoja huku wakikosa warithi – kila damu msanii mpya
wa muziki anakimbilia kwenye bongo fleva na mbaya zaidi kila mmoja
anataka kuwa mwimbaji. Hakuna anayetaka kujifunza kupiga chombo chochote
na haitashangaza miaka 20 ijayo Tanzania ikawa haina mpiga gitaa wala
ngoma.
Nadhani
alichopaswa kusema Salma Msangi ni kuwa muziki wa bendi za dansi
UNAKUFA. Bendi zimekosa ubunifu wa kwenda na wakati, ziko bendi zinapiga
aina ile ile ya muziki kwa zaidi ya miaka 10, 15 au 20 bila kujali kuwa
soko la muziki linabadilika kila wakati na kwamba walilazimika
kulifuata.
Inauma
sana unaposikiliza vipindi vya muziki wa kiafrika kama Weekend Bonanza,
Afrika Kabisa, Afro Power, Buzuki, Tanzania Stars, Afro Rhythm na
vingine vingi, vinapopiga nyimbo za wasanii wa bongo fleva badala ya
muziki wa bendi kama ilivyotarajiwa na wengi. Lakini utawalaumu vipi
watangazaji na waandaji wakati bendi zetu hazitaki kubadilika, hazitaki
kurekodi nyimbo mpya na wala hazitaki kujiuliza ni kwanini nyimbo
binafsi za wasanii wao zinapata muda wa kutosha redioni huku za bendi
zinadorora.
Kama
msanii wa bendi anaweza kutoa wimbo wake binafsi unaokidhi mahitaji ya
soko na ukapigwa redioni. ni kwanini asifanye hivyo kwenye bendi yake?
Ni wazi kuwa fikra zao hazikubali ndani ya bendi na hivyo wanaamua
kutoka kivyao vyao.
Kumbi
zinazidi kukauka mashabiki, watu wanakimbilia ‘club’ kucheza disco au
muziki wa kizazi kipya, inafika wakati hata bendi zinazopiga bure kwenye
bar hazipati mashabiki - hiyo ni dalili tosha kuwa muziki wa bendi za
dansi unakufa na kama juhudi za kuzalisha mashabiki wapya hazitafanyika,
basi ‘mauti’ kwa bendi zetu yatakuwa hayakwepeki.
Post a Comment